Monday, August 26, 2013

 
Mara baada ya bodi ya ukaguzi wa filamu na michezo ya kuigiza Bongo kuipiga ‘stop’ Muvi ya Foolish Age ya staa wa kike, Elizabeth Michael ‘Lulu’ kuliibuka maneno mengi lakini baada ya saa kadhaa serikali kupitia bodi hiyo ikamfuta machozi baada ya kuipitisha.

 
Elizabeth Michael ‘Lulu’.
Kabla ya kuruhusiwa kuendelea na maandalizi ya uzinduzi wa filamu hiyo Septemba 30, mwaka huu katika Ukumbi wa Mlimani City, Dar, kuliibuka gumzo kuwa baada ya kuzuiwa muvi hiyo Lulu alihuzunika na kutokwa chozi kabla ya kutabasamu baadaye.
Habari kutoka kwenye bodi hiyo zilieleza kuwa Lulu kupitia kampuni yake ya Proin Promotions alifika katika ofisi za bodi hiyo ili kupata kibali cha kuiachia filamu hiyo sokoni kama ulivyo utaratibu.
Bodi hiyo ilizuia filamu hiyo kuingia sokoni baada ya kukuta ina picha zilizo nje ya maadili ya Kitanzania hivyo kuhitaji marekebisho ya kuondoa vipande husika ambavyo ni vile vilivyowaonesha wahusika wakiwa na vimini vya kutisha.
 
“Kikwazo kilichoikumba filamu hiyo ni nguo fupi zilizotumiwa na waigizaji walioshiriki,” alisema mtoa habari wetu.
Kwa mujibu wa Lulu, juhudi zilifanyika kuhakikisha kuwa marekebisho yanafanyika ili kwenda na ratiba kama ilivyopangwa ambapo Ijumaa mchana alifanikiwa kuipeleka tena kwenye bodi hiyo na kupata kibali.
“Nakwambia Lulu alikuwa hoi ilipozuiliwa lakini alipoipeleka ikapitishwa, ni kama serikali ilimfuta machozi. Unajua tayari zimetumika fedha nyingi sana maana gharama za utengenezaji siyo chini ya Sh. milioni 25, ukijumlisha na gharama za uzinduzi, wee acha tu, ukiambiwa inazuiliwa lazima udate,” alisema shuhuda wa tukio hilo.
Baada ya kumegewa habari hizo, gazeti hili lilizungumza na Lulu ambapo alikiri kukutana na hali hiyo iliyomweka katika wakati mgumu lakini akafafanua kwamba anamshukuru Mungu kwa kuwa mambo yalikwenda vizuri na tayari amepata kibali hivyo uzinduzi upo palepale.
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Joyce Fissoo alisema ni kweli bodi ilizuia filamu hiyo lakini alipokamilisha marekebisho yake alipatiwa kibali.
“Hadithi ni nzuri inafaa kutazamwa na watoto wote wenye umri huo kwani ina mafunzo mengi lakini ilikuwa na vipande fulanifulani visivyo na maadili. Baada ya marekebisho alituletea tukaona ipo vizuri akapata kibali,” alisema Fissoo.
Filamu hiyo ilirekodiwa kabla ya matatizo ya kifo cha Steven Kanumba yaliyosababisha Lulu akakaa mahabusu ya Gereza la Segerea kwa takribani miezi kumi hivyo uzinduzi huo ni sehemu ya kumtambulisha rasmi staa huyo kwa mashabiki wake.
GPL

0 comments:

Post a Comment