Wabunge wa CCM Zanzibar wameibua zengwe jipya dhidi ya Makamu wa
Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad kwamba anatumia ndege ya Rais
kubebea mkaa, mihogo na ndizi kutoka Pemba kwenda Unguja.
Habari zilizopatikana kutoka ndani ya serikali ya
Mapinduzi Zanzibar zinaeleza kuwa, tuhuma hizo zilitolewa na wabunge hao
wakati wa kikao chao na Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk
Ali Mohamed Shein mwezi uliopita.
Kitendo hicho kinachodaiwa kufanyika mwezi
uliopita kimeonekena kuwakera baadhi ya viongozi wa Serikali wakiwamo
wabunge wa CCM Zanzibar, ambao wakati wa kikao hicho na Rais Dk Shein
mwezi uliopita mjini Zanzibar, walilizungumza kwa uchungu na kuomba Rais
amuonye Maalim Seif kwa kuigeuza ndege ya Rais kuwa ya mizigo.
Anayedaiwa kuibua hoja hiyo ni Mwenyekiti wa Umoja
wa Vijana Taifa (UVCCM), Sadifa Juma Khamis, ambaye alisema kuwa
kitendo hicho cha Makamu wa Kwanza wa Rais kutumia ndege hiyo kubebea
mkaa, mihogo na mikungu ya ndizi kinadhalilisha Ofisi ya Rais.
Katibu wa Wabunge wa CCM Zanzibar, Mbunge wa
Magomeni, Mohammed Chombo alipoulizwa na gazeti hili kuhusiana na suala
hilo alikiri wabunge hao kulifikisha suala hilo kwa Rais Shein.
“Tulimweleza Rais matatizo mengi likiwamo na hilo
la Makamu wa Kwanza wa Rais kutumia ndege ya Serikali kubebea mihogo na
mkaa,” alisema.
Alisema kuwa Rais aliwaambia kuwa ameyapokea malalamiko hayo na kwamba atayafanyia kazi.
Chombo alisema kuwa kwa sasa wanamsubiri Rais Shein awaite kuwapa majibu ya matatizo yao.
Baadhi ya wabunge wa CCM Zanzibar ambao
walizungumza na gazeti hili, walisema kuwa kitendo hicho ni matumizi
mabaya ya mali za umma kwa sababu kuna vyombo vingi vya usafiri
vinavyoweza kutumika kusafirishia mizigo hiyo.
Ofisa mmoja ambaye hakutaka kutajwa jina lake
kutoka Mamlaka ya Ndege za Serikali, akizungumzia utaratibu wa viongozi
wa Serikali kutumia ndege hizo, alisema viongozi wa juu wa Serikali ya
Muungano na Zanzibar hukodi ndege zao.
Alisema hajawahi kuona ndege kubebea mkaa, hata ndege ya jeshi hajawahi kuona ikibeba mkaa.
Hata hivyo, Katibu wa Wabunge wa CUF, Mohammed
Habibu Mnyaa, alisema madai hayo ya wabunge wa CCM ni siasa chafu dhidi
ya Makamu wa Kwanza wa Rais na kwamba wao wanaamini hawezi kufanya jambo
hilo.
Alisema Maalim Seif anaheshimika na ni mzoefu
katika utawala hawezi kufanya jambo hilo, wakati kuna meli ambazo
zinaweza kutumika kusafirishia bidhaa hizo kutoka Pemba kama akitaka.
“Hizi ni siasa chafu za wabunge wa CCM dhidi ya
Maalim Seif, sisi tunaamini hawezi kufanya jambo hilo hata kidogo,”
alisema Mnyaa.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais,
Fatma Abdulhabib Fereji alipoulizwa kuhusiana na suala hilo, alisema
hana taarifa na madai hayo.
“Sina taarifa na yoyote, ndiyo kwanza nayasikia kutoka kwako,” alisema.
Kaimu Katibu Mkuu wa CUF Taifa, Julius Mtatiro
alipoulizwa jana kuhusiana na suala hilo alisema kuwa Maalim Seif yuko
nje ya nchi, hata hivyo msimamo wa chama hicho ni kwamba madai hayo ya
wabunge wa CCM siyo ya kweli.
Alisema kuwa wamesikia kikao cha Wabunge wa CCM na
Rais Shein, kwamba wanachokidai kinaonyesha wazi kuwa wamekosa cha
kuwafanyia wananchi wao.
Mtatiro alisema hii siyo mara ya kwanza kwa
viongozi wa CCM kumtungia tuhuma Maalim Seif, kwani waliwahi kudai kuwa
ni mwasisi wa Kikundi cha Kiislamu cha Uamsho jambo ambalo siyo la
kweli.
“Pia viongozi haohao wa CCM waliwahi kumtupia tuhuma nyingi ambazo baadaye zinakuja kuonekana siyo za kweli,” alisema.
Alisema hata kama Maalim Seif angetumia hiyo ndege
kubebea zawadi kwani kuna ubaya gani, mbona hata viongozi wa CCM
hufanya hivyo?
“Kuna ubaya gani, viongozi wa kitaifa kubebea
zawadi, mbona hata viongozi wa CCM wakiwa katika ziara wakipewa zawadi
hubeba kwenye ndege?”
Huu ni msukosuko mwingine katika serikali ya umoja
wa kitaifa. Hivi karibuni Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar,
iliingia kwenye msukosuko baada ya viongozi wake kutofautiana kuhusu
muundo wa Muungano. Maalim Seif aliwahi kunukuliwa akisema anataka
serikali ya mkataba, kauli ambayo ilipingwa na viongozi wengine hususan
kutoka CCM.
Wakati makamu huyo wa kwanza akisema hivyo, Rais
Shein alisikika akisema anataka muundo wa sasa wa serikali mbili. Hata
hivyo, wiki iliyopita Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Othman Masoud Othman
alisema kuwa mwarobani wa Muungano ni kuwa na serikali tatu.
0 comments:
Post a Comment